Na Wilbert Molandi
KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Liewig, ameridhishwa na umbile, nguvu na stamina ya beki wa kati, Juma Nyosso (pichani), huku akiahidi kumpa mechi ya kuangalia uwezo wake.
Beki huyo amerejea hivi karibuni kwenye kikosi cha kwanza, baada ya kushushwa hadi timu ya vijana kwa kile kilichodaiwa kuwa kiwango chake kilishuka ingawa hakucheza kwenye kikosi hicho.
Juzi beki huyo alikuwa mazoezini na wenzake kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, Liewig alisema licha ya beki huyo kuwa na sifa hizo zote zinazostahili, haitoshi kujiridhisha na badala yake atampa mechi kadhaa za kumuangalia kabla ya kumpa namba ya kudumu kwenye kikosi chake.
“Nimefurahi kumuona Nyosso kwa mara ya kwanza, nimemuangalia kwa muda mchache, nimeridhishwa na umbile, nguvu na stamina yake, ni vitu ambavyo anastahili kuwa navyo beki wa kati.
“Lakini hivyo vyote haviniridhishi ili nimpange kwenye kikosi cha kwanza, nahitaji kumuangalia akiwa uwanjani akicheza ili kuona uwezo wake zaidi kabla ya kumpa nafasi ya kucheza.
“Ujio wake kwenye timu utaleta changamoto kwa upande wa mabeki wa kati ambao ni Shomari Kapombe, Musa Mudde na Komambil Keita. Ninaamini nitakuwa na wigo mpana wa kuchagua mabeki wazuri wa kati wenye uwezo,” alisema Liewig.
0 comments: